emblem

The United Republic of Tanzania

National Social Security Fund (NSSF)

We Build Your Future

News

​WAZIRI MKUU AAGIZA MAKONTENA YENYE MITAMBO YA KIWANDA CHA SUKARI MBIGIRI YALIYOKWAMA BANDARINI YATOKE MARA MOJANa MWANDISHI WETU

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Watanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amewaagiza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama pamoja na Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tixon Nzunda wakutane kwa haraka ili wafanye maamuzi ya utoaji wa makontena 21 yenye mitambo mbalimbali ya ujenzi wa kiwanda cha sukari Mbigiri yaliyokwama katika bandari ya Dar es Salaam.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo baada ya kutembelea mradi wa shamba la miwa Mkulazi na kupokea taarifa ya ujenzi wa kiwanda cha sukari Mbigiri kilichopo mkoani Morogoro, ambapo alielezwa kuwa baadhi ya makontena yenye mitambo ya kiwanda hicho yamekwama katika bandari ya Dar es Salaam.

“Katibu Mkuu (Ofisi ya Waziri Mkuu) upo hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, ndiye anayeisimamia NSSF (Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii) pamoja na mradi huu, Waziri wa Fedha na Mipango ambaye ndiye mwenye mamlaka na TRA wakutane kwa haraka tunataka kuona makontena yote yanakuja hapa na kiwanda kuendelea kujengwa ili kukidhi lengo la Serikali la kujitosheleza katika mahitaji ya sukari nchini liweze kukamilika,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwa sasa mahitaji ya sukari ya mezani ni zaidi ya tani 360,000 ambapo uzalishaji wa sukari nchini ni tani 280,000 mpaka tani 290,000 hivyo bado kuna pengo la mahitaji ya sukari tani 70,000.

Alisema hakuna jambo ambalo litakwama kwani mitambo hiyo imeletwa kwa ajili ya kujenga kiwanda, hivyo kama kuna suala la kodi zibainishwe ili ziweze kulipwa na mitambo iletwe Mbigiri.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema hawataupa nafasi ucheleweshwaji wa mitambo hiyo usiokuwa na ulazima na alimuagiza Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga kumfikishia salamu Waziri Jenista kwamba wakae na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Nchemba wafanye maamuzi ya kutoa makontena hayo na taratibu nyingine ziendelee ili ujenzi wa kiwanda hicho usikwame.

Alisema kwa kufanya hivyo Bodi haitapata hasara kwa mkandarasi anayejenga kiwanda hicho kwa kumcheleweshea hatua alizojipangia za ujenzi wake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema kupitia ziara ya Waziri Mkuu wamefarijika kwani nia ya dhati ya Serikali ambayo inataka kiwanda hicho kianze kazi ya uzalishaji sukari haraka iwezekanavyo inaonekana.

“Tunaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia kwa Waziri Mkuu aliyeagiza yale makontena yenye vifaa vya viwanda yatolewe mara moja bandarini na shughuli za ujenzi ziendee. Hili ni jambo kubwa na zuri sana kwetu sote” alisema.

Mshomba alisema NSSF kama wamiliki wa kampuni ya Mkulazi na watoa fedha wakubwa wamepokea uamuzi huo kwa furaha, kwani kwa kufanya hivyo uzalishaji utaanza na wataanza kurudisha fedha mapema.

Naye, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Msepwa Abdalla Omar, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi wa Shirika la Magereza, alisema ziara ya Waziri Mkuu imewapa tumaini jipya kwani sasa kiwanda kinaenda kukamilika, uzalishaji utaanza na matarajio ya Serikali pamoja na wabia wa kiwanda hicho ambao ni NSSF na Jeshi la Magereza kupitia kampuni tanzu ya Mkulazi yatapatikana.