Mpango wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF ulianza kama Idara ya Serikali mwaka 1964 kabla ya kuanzishwa kama Shirika la Taifa la Akiba ya Wafanyakazi (NPF) kwa Sheria Na. 36 ya mwaka 1975. Shirika hili liliendelea hadi pale Serikali ilipopitisha Sheria Na. 28 ya mwaka 1997 iliyoanzisha Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii kama mpango kamili wa hifadhi ya jamii unaozingatia kanuni za kimataifa za hifadhi ya Jamii.
Mabadiliko hayo yameiwezesha NSSF kutoa mafao mengi na bora zaidi yakiwemo mafao ya pensheni ambapo kabla ya hapo mfumo wa akiba wa NPF ulikuwa unatoa mafao ya uzeeni kwa njia ya mkupuo. Mafao hayo yalikuwa ni hafifu na machache sana.
Mpango wa NSSF hutoa mafao ya aina saba (7) ambayo yamegawanyika katika makundi makuu mawili;
(a) Mafao ya muda mrefu
- Pensheni ya Uzee
- Pensheni ya Ulemavu na
- Pensheni ya Urithi
(b) Mafao ya muda mfupi
- Mafao ya Uzazi
- Mafao ya kuumia kazini na magonjwa yatokanayo na kazi
- Msaada wa Mazishi na
- Mafao ya Matibabu (SHIB)
Shirika pia hulipa mafao ya kujitoa uanachama kwa mfumo wa akiba kwa mwanachama aliyeondoka katika ajira kwa sababu mbali mbali kabla hajatimiza umri wa kustafu na ikiwa hajapata kazi nyingine kwa zaidi ya miezi sita.