News Archive

Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii - NSSF
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni Shirika la umma ambalo lilianzishwa mwaka 1967 Kama Idara inayoshughulikia pensheni ndani ya Wizara ya Kazi. Idara hii iliboreshwa zaidi mwaka 1975 na kubadilishwa kuwa taasisi kamili (NPF) iliyokuwa na jukumu la kushughulikia mafao kwa wafanyakazi baada ya kustaafu. Maboresho zaidi katika sheria yalifanyika mwaka 1997, ambapo NPF ilibadilishwa na kuwa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ili kuongeza wigo wa mafao yanayotolewa.

Majukumu makubwa ya NSSF ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, kuwekeza michango hiyo na kulipa mafao. Mafao yanayotolewa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii yamegawanyika katika makundi mawili, makundi hayo ni mafao ya muda mrefu na mafao ya muda mfupi. Mafao ya muda mfupi ni; Fao la Matibabu, Fao la Uzazi, Fao la Kuumia Kazini na msaada wa mazishi. Mafao ya muda mrefu ni Pensheni ya Ulemavu, Pensheni ya urithi na Pensheni ya Uzee.

Uwekezaji wa NSSF katika Viwanda
Mbali na lengo la kutunza thamani ya michango ya wanachama, uwekezaji unaofanywa na Shirika pia unalenga kuchochea ukuaji wa shughuli mbali mbali za uchumi na kijamii ambazo pia huongeza ajira, kipato na kuinua kiwango cha maisha ya watanzania walio wengi.  Moja ya maeneo ambayo Shirika huwekeza ni pamoja na uanzishaji, uendelezaji na uimarishaji wa viwanda katika sekta mbali mbali za kiuchumi. Uwekezaji huu wa Shirika umeviwezesha viwanda hivi kuongeza uzalishaji wa bidhaa na  kuchangia katika ongezeko la ajira na kipato. Uwekezaji huu pia umechangia kuongezeka kwa pato la Serikali kutokana na tozo za kodi mbali mbali zinazohusiana na viwanda hivi.

Uwekezaji wa NSSF katika Viwanda kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano
Katika kipindi cha awamu zilizopita, Shirika liliwekeza katika viwanda kwa njia mbalimbali. Njia hizo ni pamoja kuchangia mtaji wa kudumu katika kiwanda (equity investment) au kwa kutoa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa viwanda hivi. Viwanda vilivyofaidika na uwekezaji huu katika kipindi hiki ni pamoja na Kiwanda cha Sukari cha Kagera, Kiwanda cha Nguo (21st Century Texitles Limited) – Morogoro, Kiwanda cha Bidhaa zitokazo na Mkonge (Katani Limited) – Tanga, Kiwanda cha Vifaa vya Hospitali (Meditech Limited) – Dar es Salaam, Kiwanda cha Cement – (Dar es Salaam Cement Limited) Dar es Salaam, mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, n.k.

Uwekezaji pia ulitekelezwa kupitia ununuaji wa hisa katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE), Shirika liliwekeza katika Kiwanda cha Kuchakata Gesi (Tanzania Oxygen Limited) – Dar es Salaam, Kiwanda cha Bia (Tanzania Breweries Limited) – Dar es Salaam, Kiwanda cha Sigara (Tanzania Cigarette Company) – Dar es Salam, kiwanda cha Majani ya Chai Tanzania – (Tanzania Tea Packer), Kiwanda cha Sementi cha Simba (Tanzania Cement Company) – Tanga na Kiwanda cha Sementi cha Twiga (Tanzania Portland Cement Company Limited) – Dar es Salaam.

Shirika liliweza kunufaika kutokana na uwekezaji uliofanywa kwa kupata gawio lililokuwa likitolewa kutokana na faida iliyopatikana. Aidha, mashirika haya yaliweza kuendeleza shughuli zao kutokana na mitaji waliyopatiwa na hivyo kuchangia katika pato la taifa na kuwezesha kutoa ajira kwa wananchi baada ya kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji. Serikali kwa upande mwingine iliweza kunufaika na kodi mbali mbali kutoka katika mauzo ya bidhaa zilizozalishwa na mishahara iliyokuwa ikilipwa kwa watumishi wake. Viwanda hivi pia vilisaidia kuongeza wanachama waliokuwa wakujiunga na NSSF na mifuko mingineyo.

Uwekezaji wa NSSF katika Viwanda Wakati wa Awamu ya Tano
Shirika limeitikia kwa vitendo wito wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Joseph Pombe John Magufuli wa kufufua, kuanzisha, kuendeleza na kuimarisha viwanda ili kuliwezesha taifa kukuza uchumi wake na kufikia kiwango cha uchumi wa kati  na wenye manufaa zaidi kwa watanzania wote.

Kwa kuzingatia Sera ya Uwekezaji ya Shirika na Mwongozo wa Uwekezaji kwa Mashirika ya Hifadhi ya Jamii unaotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa kushirikiana na Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Shirika linaendelea kuwekeza katika viwanda kwa kutoa mtaji wa kudumu  na mikopo kwa ajili ya kufufua viwanda vilivyo kuwa vimesimama pamoja na kuanzisha viwanda vipya.

Uwekezaji wa Shirika katika viwanda hivi unazingatika umuhimu na mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa kupitia uzalishaji, uongezaji wa thamani, uzalishaji wa ajira na kipato kwa wananchi, kuongezeka kwa makusanyo ya kodi kwa Serikali, uokoaji wa fedha za kigeni, kuongeza fedha za kigeni kupitia uuzaji nje wa baadhi ya bidhaa na utunzaji wa mazingira.

Viwanda vya Kusaga Nafaka na Kukamua Mafuta ya Alizeti
Kwa kuzingatia umuhimu na mahitaji makubwa ya nafaka na mazao mengine katika taifa na nchi nyingine hususani zile zilizoko katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na  Kati na Kusini mwa Jangwa la Sahara, Shirika kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), limewekeza katika  mradi wa kufufua na kuboresha viwanda vya kusaga nafaka ambavyo awali  vilikuwa vinamilikiwa na Shirika la Taifa la Usagishaji (NMC). Mradi huu unahusisha ufufuaji wa viwanda vilivyopo mkoani  Iringa, Dodoma, Arusha na Mwanza.

Kwa kuanzia, Shirika limetoa mkopo wa shilingi bilioni 3.67 kwa ajili ya ununuzi wa kinu cha kusaga mahindi na mashine ya kukamua mafuta ya alizeti.  Mashine hiyo mpya ya kisasa inayo uwezo wa kusaga tani 60 za nafaka kwa siku. Pia sehemu ya fedha hizi zitatumika kununua mashine ya kukamulia mafuta kutoka katika mbegu za alizeti, mashine hii itakuwa na uwezo wa kukamua tani13 za alizeti kwa siku.
Utekelezaji wa mradi huu uliopo Dodoma uko katika hatua za manunuzi. Usagaji wa nafaka na ukamuaji wa mafuta katika kiwanda hiki cha Dodoma unategemewa kuanza mwanzoni mwa  mwaka  ujao wa fedha.


Faida Tarajiwa
Vinu hivi ya kusaga na kukamua mafuta vinatarajiwa kuongeza thamani ya mazao ya wakulima katika mikoa ya kanda ya kati ya Dodoma, Singida na Manyara ambapo mazao yao ya mahindi, alizeti na mengineyo yatanunuliwa na CPB kwa bei nzuri na kwa malipo ya wakati kwa ajili ya kiwanda hiki. Inatarajiwa zaidi ya wakulima 10,000 watafaidika na mradi huu. Aidha ajira za kudumu zipatazo 250 zitazalishwa na  zaidi ya watu 6,000 wanatazamiwa kunufaika kwa njia moja ama nyingine na mradi huu kutokea hatua za ulimaji wa mazao haya hadi kufikia kwa mlaji.

Matarajio ya Baadaye
Baada ya kukamilika kwa shughuli za ufufuaji  wa vinu vya kusaga nafaka vilivyopo mkoani Dodoma na kuweka mashine za kukamua mafuta, Shirika pamoja na CPB wanatarajia kuboresha vinu vilivyopo mkoani Iringa, Mwanza na baadaye Arusha

Kiwanda cha Kutengeneza Viuadudu vya Kuua Vimemlea vya Mbu
Ugonjwa wa malaria ni moja ya magonjwa yanayouwa watu wengine kila mwaka hapa Tanzania, Africa na katika nchi nyingine ulimwenguni. Takwimu zinaonyesha zaidi ya watu 200,000 hufariki hapa Tanzania kila mwaka kwa ugonjwa huu. Taifa linatumia fedha nyingi kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huu. Fedha hizo hutumika kwa ajili ya kununulia dawa za kutibu ugonjwa huu pamoja na kufanya tafiti mbali mbali juu ya dawa mahiri za kutibu malaria pia juu ya uwezekano wa kuwapunguza au kuwatokomeza kabisa mbu ambao ndio chanzo kikuu cha ugonjwa huu.

Fedha hizi pia hutumika katika program mbali mbali za kuelimisha umma kwa juu ya njia sahihi za kujikinga na ugonjwa huu, kununua na kugawa dawa za kuuwa vimemlea vya mbuu, kununua na kugawa vyandarua vyenye dawa. Kwa kudhiti ugonjwa huu, Taifa litaokoa fedha nyingine na kuzitumia kwa matumizi mbadala ya maendeleo.

Juhudi za Serikali Kujenga Kiwanda
Katika jitihada za kudhibiti ugonjwa huu katika kipindi kifupi na kwa gharama nafuu zaidi, Serikali kwa kushirikia na Serikali ya Cuba, iliamua kujenga kiwanda cha kuzalisha viuadudu vya kuulia vimelea vya mbu. Kiwanda hiki kinajulikana kama TANZANIA BIOLARVICIDE LIMITED na kipo Kibaha, Mkoani Pwani.  Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) ndiye msimamizi mkuu wa mradi huu wakati Kampuni ya LABIOFARM kutoka Cuba ndiye yenye haki miliki na teknolojia ya uzalishaji wa viuadudu hivyo. Kiwanda hicho kimejengwa katika kiwanja Na. 24 kilichopo katika  eneo la  TAMCO wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Kiwanda kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita za viuadudu husika kwa mwaka. Kiwanda kimekamilika na kimeanza uzalishaji mwishoni mwa mwaka 2016.  Katika ujenzi wa kiwanda hiki, Serikali imegharimia asilimia 75% ya gharama zote za ujenzi na NDC imechangia asilimia 25%.


Ushiriki wa NSSF
Kwa kupitia NDC, Shirika limetoa mkopo wa muda wa kati wa Dola za Kimarekani 2.1 ikiwa na mtaji wa kuendeshea kiwanda hiki.

Faida za kiwanda
Kiwanda kimeanza kuzalisha dawa ambayo inatumika kuuwa vimelea vya mbu vilivyopo katika hatua ya lava.upatikaji wa dawa hii hapa nchini kunaokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza dawa hizo knje ya nchi.

Mauzo ya dawa hizi kwa mataifa ya nje kutaliingizia taifa fedha za kigeni ambazo zitatumika katika mipango mingine ya maendeleo.  Aidha, kupungua kwa ungonjwa wa malaria na vifo vitokanavyo na ugonjwa huu kutaliongezea taifa nguvu kazi na kutaongeza tija zaidi katika ukuaji wa uchumi na shughuli nyinginezo.

Hadi sasa kiwanda kimetoa ajira za kudumu 135 kwa watanzania na hivyo kupunguza tatizo la ajira na pia kuongeza kipato na kuboresha zaidi viwango vya maisha vya watanzania.

Matarajio ya Baadaye
Kiwanda kinatarajia kuendelea kuongeza uzalishaji wa dawa hizi ili kutosheleza mahitaji ya ndani ya nchi lakini pia kuzalisha ziada kwa ajili ya nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Afrika na nchi nyingine ulimwenguni. Tayari baadhi ya nchi za Afrika, ikiwemo Niger, Rwanda zimeanza kufaidika na dawa hii. Kiwanda kinafanya juhudi zaidi za kuhamasisha kila wilaya kutumia dawa hizi na pia kutangaza dawa hii kwa mataifa mengine juu ya upatikanaji wa dawa hizi muhimu katika mapambano dhidi ya ugonjwa hatari wa malaria.

Viwanda Vipya vya Kuzalisha Sukari
Sukari ni moja ya bidhaa muhimu kwa mahitaji ya nyumbani na viwandani. Kwa muda mrefu Taifa limekuwa na upungufu wa bidhaa hii. Hali inaonyesha kuwa endapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa kuanzisha viwanda vingi zaidi vya kuzalisha sukari au kuongeza uwezo wa viwanda vilivyopo, basi upungufu wa sukari utakuwa mkubwa zaidi kadri  idadi ya watu  inavyoongezeka.

Kwa wastani mtu mmoja katika nchi yetu anakadirwa kutumia wastani wa sukari kilo 12 kwa mwaka. Hivyo mahiji ya sukari kwa sasa ni zaidi ya tani 641,000 kwa mwaka wakati uwezo wa kuzalisha wa viwanda vitano vilivyopo nchini ni chini ya tani 400,000 kwa mwaka. Taifa lina lazimika kuagiza kutoka nje kiasi kibwa cha cha sukari ili kukidhi mahitaji haya.

Ushiriki wa NSSF Katika Ujenzi wa Viwanda Vya Sukari
Katika jitihada za kupunguza tatizo la upatikanaji wa uhakika wa sukari nchini, pia kwa kuzingatia ukubwa wa tatizo hili katika siku za baadae endapo hatua stahiki hazitachukuliwa sasa na pia kwa nia ya kuokoa kiasi kikubwa cha fedha za kigeni zinazotumika kuagizia sukari kutoka nje ya nchi, Shirika limeamua kushiriki moja kwa moja katika juhudi za kuanzisha viwanda vipya na vya kisasa vya uzalishaji wa sukari.

Katika juhudi hizi, Shirika limeingia ubia na Mfuko wa Pensheni wa PPF na kwa pamoja wameanzisha kampuni tanzu ya Mkulazi Holding Company Limited (MHCL) ambayo ina jukumu la kuanzisha na kusimamia miradi mbali mbali ya uzalishaji wa sukari. Kwa sasa Shirika hili (MHCL) linatekeleza miradi miwili ya ujenzi wa viwanda vya sukari ambavyo kwa pamoja vitazalisha jumla ya tani 230,000 za sukari kwa mwaka.

Mradi wa Kiwanda Cha Sukari Cha Mkulazi I
Mradi huu unaohusisha ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha sukari ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 200,000 za sukari kwa mwaka. Pia kiwanda hiki kitazalisha bidhaa nyingine zitokanazo na ukamuaji wa miwa ikiwemo chakula cha mifungo na gesi ya ethano na gesi ya ukaa (kaboni dioksaidi) ambayo inaweza kutumiwa na viwanda vingine vya vinywaji.
Mradi huu unatekelezwa katika eneo la ukubwa wa hekta 63,227 liliopo eneo la Mkulazi, Ngerengere, mkoani Morogoro ambapo lipo umbali wa kilometa 195 kutokea Manispaa ya Morogoro na kilometa 75 kutoka eneo la Ubena-Zomoni katika barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro.

Mradi pia utahusisha ulimaji wa miwa katika eneo lisilopungua hekta 28,000 ambapo kilimo cha kutegemea mvua kitaimarishwa kwa kutumia njia za kisasa za umwagilia. Mradi pia unatazamiwa kujumuisha ulimaji wa miwa kwa kutumia wakulima wadogo wadogo (outgrowers) ambao watawezeshwa kulima miwa kwa ufanisi mkubwa kupitia huduma za ushauri kutoka kwa watalaam wa kilimo cha miwa wa mradi. Miwa yote itakayolimwa na wakulima hawa itanunuliwa na kiwanda.

Kwa upande mwingine, hekta 20,000 zimetegwa kwa ajili mazao ya nafaka kama vile  alizeti na mtama kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi na ziada kuuzwa nje ya nchi.

Ubora wa eneo la Mradi
Kiuchumi eneo la Mkulazi liko kati ya reli ya kati kwenye kituo cha Ngerengere pamoja na Reli ya TAZARA kupitia kituo cha Kidunda  na pia linafikika kwa barabara katika umbali wa kilometa 75 kutoka barabara kuu ya lami ya Dar es Salaam – Morogoro. Hivyo uwekezaji katika eneo hilo utafanya usafirishaji wa malighafi na bidhaa kuwa rahisi na wa gharama nafuu.

Faida za Kiwanda
Kukamilika kwa mafanikio kwa mradi huu kutaongeza upatikanaji wa sukari nchini kwa  kiasi cha tani 200,000 zaidi na hivyo kupunguza uagizaji wa sukari kutoka nje na hivyo kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza sukari.  

Pia mradi utatoa fursa za ajira za moja Kwa moja zisizopungua 4,000 na zile za muda takriban 40,000. Aidha inategemewa kuwepo kwa ajira zisizo za moja kwa moja zisizopungua 100,000. Ajira hizi zitajumuisha watu watakao ajiriwa katika sehemu ya utawala, kiwanda, ndani na nje ya shamba.

Mradi huu sio tuu utaongeza kipato kwa mifuko hii miwili kutokana na uwekezaji uliofanyika na ongezeko la wigo la wanachama, bali pia utaongeza pato kwa Serikali kuu na serekali za wilaya na vijiji kupitia tozo za kodi.

Zaidi mradi utarudisha sehemu ya mafanikio yatakayopatikana  kwa wananchi ambapo miradi inayojumuisha uboreshaji wa miundombinu mfano barabara na uimarishaji wa huduma za afya na elimu.

Kuanza kwa Shughuli za Uzalishajiwa Sukari
Uzalishaji katika kiwanda hiki unatazamiwa kuanza mwaka 2019. Katika muda huu maandalizi ya shamba la miwa na miundo mbinu ya umwagiliaji inaendelea. Aidha kampuni ya Mkulazi imekwisha kamilisha tathmini mbalimbali za shamba zikiwemo tathimini ya udongo..

Kiwanda cha Sukari cha MKulazi II
Hiki ni kiwanda cha sukari kinajengwa eneo la Mbigiri, Dakawa, Mvomero, mkoani Morogoro umbali wa KM 55 kutoka Manispaa ya Morogoro.

Uazishwaji wa kiwanda hiki ni matokeo ya ushirikiano wa Kampuni ya Mkulazi Holding na Idara ya Uzalishaji Mali ya Magereza (Prisons Corporation Sole -PCS) ambayo inamiliki eneo lenye ukubwa wa ekari 12,000 ambalo mradi huu unatekelezwa.  Mkataba wa Maelewano kati ya MHCL na PCS ulisainiwa tarehe tangia 24 Februari 2017.

Lengo la mradi huu ni kuanzisha tena shughuli za uzalishaji wa sukari katika eneo hili. Hapo awali eneo husika lilikuwa likizalisha sukari lakini kutokana na uchakavu wa mashine, uzalishaji huu ulisima mwaka 1998.

Kiwanda hiki kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 30,000 za sukari kwa mwaka na tani zaidi ya 9,000 za chakula cha mifungo kutokana na mabaki ya miwa. Mashine mpya na za kisasa za uzalishaji sukari zitafungwa katika kiwanda hiki ili kuhakikisha tija inapatikana.

Ili kufikia lengo hili la uzalishaji sukari, kiwanda kitakamua miwa iliyolimwa na kiwanda chenyewe pamoja na miwa itakayolimwa na wakulima wa miwa wadogo wadogo (outgrowers) walio karibu na kiwanda. Mradi huu pia utajumuisha ujenzi wa  ghala za kutunzia sukari, majengo ya ofisi, nyumba za wafanyakazi wa kudumu na hosteli kwa ajili ya wafanyazi wa msimu. Kwa upande mwingine, mradi unajumuisha ununuaji wa zana mbalimbali za kilimo zikiwemo matrekta, magari ya kubebea miwa kutoka mashambani na utengezaji wa miundo mbinu ya uwagiliaji katika mashamba ya miwa.

Faida za Kiwanda
Kiwanda hiki kinatarajiwa kuanza uzalishaji mwezi Juni 2018 na kitatoa ajira za kudumu 245. Aidha, kutakuwa na ajira za muda mfupi hasa wakati wa ujenzi wa kiwanda, uandaaji na upandaji wa miwa ambapo inategemewa ajira zisizopungua 10,000 zitazalishwa kupitia mradi huu. Kiwanda hiki pia kitazalisha umeme usio pungua Megawati 2 kwa ajili ya matumizi yake kwa kutumia mabaki ya miwa.

Hitimisho
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ni mshriki wa muda mrefu katika juhudi za uendelezaji wa viwanda nchini. Kwa kupitia uzoefu lilionao litekeleze kwa vitendo mwongozo wa Serikali wa kuongeza na kuimarisha viwanda nchini. Katika utekelezaji wa mwongozo huu, NSSF imejikita katika kuanzisha na kuendeleza viwanda ambavyo vitasaidia Taifa kukidhi mahitaji yake ya muhimu, pia vile ambavyo vitaweza kuzalisha ajira za muda mrefu kwa wingi, kuongeza thamani ya mazao, vyenye mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii na zaidi katika kuipatia Serikali mapato kwa ajili ya kuendeleza huduma mbali mbali kwa wananchi walio wengi.

Frequently Asked Questions

 • Nawezaje kuwa mwanachama wa NSSF? +

  Tafadhali fika katika ofisi yoyote ya NSSF iliyo karibu yako kwa zoezi la uandikishaji ukiwa na picha moja ya passport Read More
 • Napataje taarifa ya Michango yangu? +

  Kupata taarifa ya Michango, unafanya ifuatavyo : a) Sajili Tuma neno sajili,acha nafasi, weka namba yako ya uanachama. Tuma kwenda namba Read More
 • Je nifanyeje endapo michango yangu haionekani katika taarifa za akaunti yangu? +

  Tafadhali fika ofisi ya NSSF iliyo karibu nawe ili kujua sababu ya kutoonekana kwa michango yako na kuelekezwa utaratibu wa Read More
 • Je narekebishaje michango yangu? +

  Michango ya mwanachama itarekebishwa kulingana na sababu zinazopelekea kutoonekana kwa michango hiyo katika taarifa ya michango. Ofisi husika itakupa muongozo zaidi. Read More
 • Je mwanachama anayesafiri anaweza kumwachia mtu au ofisi imfatilie madai na kuchukua malipo yake?? Kwa utaratibu gani?? +

  Ndio, mwanachama anaruhusiwa kwa kujaza fomu za mandate (NSSF 22) zilizothibitishwa na mwanasheria na kufata taratibu zote za kisheria zilizoainishwa Read More
 • 1
 • 2
 • 3
 • 4